Mswaada unaolenga kuoanisha sheria za
ndoa nchini Kenya umewasilishwa bungeni.Baadhi ya mabadiliko yaliopendekezwa
katika mswada huo ni pamoja na kuhalalisha ndoa za wake wengi mbali na
kuziimarisha sheria zote saba za ndoa.
Mapendekezo mengine ambayo huenda
yakazua hisia kali ni yale ya kugawa mali iliochumwa katika ndoa pamoja na
adhabu ya wanaume ambao huvunja ahadi zao za kuwaoa akina dada.
Hatahivyo akina dada wana kibarua cha
kuthibitisha mahakamani iwapo ahadi hiyo ilitolewa na kuvunjwa.
Licha ya kuwa ndoa za WAKE wengi
hutekelezwa na jamii nyingi nchini kenya, bado hazijahalalishwa.lakini katika
mswada huu mpya ,ndoa hizo zimependekezwa.Hatahivyo mwanamume ambaye angependa
kuingia katika ndoa hizi ni sharti aweke wazi majina yote ya wake zake mbele ya
msajili wa ndoa pamoja na rukhsa aliyopata kutoka kwa wake hao.
Vilevile wake hao pia watalazimika kutia
sahihi makubaliano kwamba wako tayari kumruhusu mume wao kuongeza mke
mwengine.Makubaliano hayo yatalazimika kumfikia msajili wa ndoa siku 21 kabla
ya harusi hiyo.hatua hiyo inalenga kupunguza migogoro ya ndoa inayotokana na
kifo cha mwanamume aliyeoa.
Hatahivyo mswada huo unashinikiza kwamba
ni sharti mtu aingie katika ndoa hiyo kupitia dini ya kiislamu au sheria za
ki-mila.Wale ambao wanataka kuoa au ambao wameoa kupitia sheria za
ki-kristo,ki-hindu ama sheria za kawaida hawatakubaliwa kuongeza wake zaidi ya
mmoja.
Mabadiliko mengine ni yale ya walio
katika ndoa kugawanya mali waliochuma kwa usawa bila kujali ni nani
aliyechangia pakubwa kupata mali hiyo.
licha ya mswada wa hapo awali
kupendekeza kufutiliwa mbali kwa mahari ,mswada huu mpya uko wazi kuhusu hilo
na kwamba mtu anaweza kulipa Mahari au la akizingatia desturi za jamii
yake.Mswada huo pia unawalinda wahusika dhidi ya kulazimishwa kuoa.
Hii ina maana kwamba wapenzi walioachana
wana uwezo wa kwenda mahakamani kutokana na ahadi za uwongo zilizotolewa na
wapenzi wao.
Aidha wanaume au wanawake walio-ahidiwa
kuolewa na ahadi hiyo kuvunjwa watahitaji kulipwa fidia.hatahivyo mwanamke
atalazimika kudhihirisha mahakamani iwapo hatua hiyo ilimuathiri. Harakati za
kuwasilisha mswada kama huo hapo awali zimegonga mwamba bungeni, huku wabunge
wengi wa kiume wakisema kuwa unawapa wanawake uwezo mkubwa katika ndoa.
No comments:
Post a Comment