KONA za mji wa Mbeya zimezizima kwa minong’ono baada ya kuibuka kwa taarifa za mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa kujifungua mtoto ambapo inadaiwa kuwa mimba hiyo alipewa na kaka yake mwenye umri wa miaka 18.
Binti huyo aliyekuwa akiishi na mama yake mkubwa alipewa mimba hiyo na kaka yake ambaye ni mtoto wa mama yake mkubwa na alipobainika kuwa mjamzito alifungiwa ndani na mama yake huyo ili wananchi wasibaini tukio hilo.
Mtoto huyo ambaye alikuwa akisoma Shule ya Msingi ya Ndora iliyopo Kijiji cha Salala, Mji Mdogo wa Mbalizi Mbeya, alisema kaka yake alikuwa akimtishia kwa kisu na kumlazimisha kufanya naye ngono, jambo ambalo anadai lilimfanya akubalie naye.
Anasema alisimamishwa kwenda shule na mama mkubwa huyo baada ya mama yake mzazi kufariki dunia.
Aliongeza kuwa anamshukukru Mungu kwa kujifungua salama mtoto wa kike, lakini mama yake huyo alishindwa kumpa huduma nzuri, hivyo kupata vidonda sehemu za siri vilivyosababisha kutokwa usaha mara kwa mara.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Pipeline eneo la Mbalizi, Asifiwe Mwakalonge, taarifa hizo alizipata Januari 2, mwaka huu kutoka kwa Mjumbe wa Kitongoji hicho, Kennedy Maniamba.
Alidai kuwa mjumbe huyo alimkuta binti huyo mdogo akienda kuchota maji Mto Mbalizi huku akichechemea na kuvuja usaha ambapo baada ya kumhoji ndipo alipopata taarifa hizo za kusikitisha.
Lakini cha kushangaza mama huyo hakuonesha nia yoyote ya kumpeleka binti huyo hospitalini.
Baada ya polisi kupata taarifa hizo walimlazimisha kumpeleka hospitali na baada ya kufika huko alidanganya umri akidai kuwa ana miaka 14.
Mtoto huyo aliendelea kusisitiza umri wake huo na aliyempa mimba ni kaka yake. Hata hivyo, mama anayeishi naye alikanusha taarifa hizo akidai kuwa mimba hiyo alipewa na kijana ambaye yuko mbali kwa sasa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alipopigiwa simu na gazeti hili kuthibitisha tuhuma hizo alisema yupo kikaoni na atatoa taarifa hizo baadaye leo.
Source: Darleo
No comments:
Post a Comment