Mama Kanisa anajitahidi kuwa makini, ili kuwasaidia vijana waweze kufurahia maisha ya ujana wao na hatimaye, waweze kujiandaa kikamilifu katika kutekeleza majukumu mbali mbali ndani ya familia na jamii kwa ujumla, kwa kukazia tunu na maadili mema kama msingi bora wa maisha.
Ujana ni kipindi cha mpito, lakini fainali iko uzeeni ndivyo wanavyosema waswahili. Ngono, ulevi wa kupindukia na matumizi haramu ya madawa ya kulevya ni kati ya vishawishi vikubwa vinavyoyaandama maisha ya vijana, sehemu mbali mbali za dunia.
Baraza la Maaskofu katoliki nchini Ireland, wameandaa mbinu mkakati utakaowasaidia vijana kuepukana na madhara yanayotokana na ulevi wa kupindukia, matumizi haramu ya madawa ya kulevya na ngono kabla ya ndoa, ili kuwajengea misingi ya utu wema kuanzia sasa. Hili ni jukumu la Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Familia na waamini maparokiani wametakiwa kujifunga kibwebwe ili kupambana na ulevi wa kupindukia na matumizi haramu ya madawa ya kulevya. Wazazi na jamii inafahamu mienendo ya watoto wao mtaani, wakiamua kushirikiana na Kanisa, vitendo hivi vinavyotishia uhuru, maisha na tunu bora za kikristo na kijamii vitaweza kudhibitiwa.
Wazazi wawaelimishe watoto wao kwa mifano mizuri ya maisha madhara ya ulevi wa kupindukia na ngono za utotoni. Kila kitu kina wakati wake, vijana wajifunze kuvuta subira, hata wakati mwingine wasukumwe na dhamira nyofu kusema "NO TIME".
Watoto na vijana wanayo haki ya kukua na kulelewa katika mazingira safi na salama, wakilindwa dhidi ya matumizi haramu ya madawa ya kulevya na ulevi wa kupindukia.
No comments:
Post a Comment